SERiKALI kupitia wizara
ya nchi ofisi ya rais tawala za mikoa na serikali za mitaa TAMISEMI imesema
itahakikisha inatoa ajira za watendaji wa vijiji na kata kutoka katika chuo cha
serikali za mitaa cha HOMBOLO kutokana na wahitimu hao kuwa na uwezo mkubwa wa
kusimamia mambo mbalimbali katika jamii kupitia elimu wanayoipata.
Kauli hiyo
imetolewa na waziri wa nchi ofisi ya rais tawala za mikoa na serikali za mitaa TAMISEMI
Selemani Jafo wakati akizungumza katika uzinduzi wa mnara wa Magufuli (MAGUFULI
SQUARE) uliojengwa katika chuo cha serikali za mitaa kilichopo kata ya Hombolo
mkoani Dodoma.
Waziri Jafo amesema
wanafunzi wanaotoka katika chuo hicho ndio hasa watakaokwenda kufanya kazi
katika mamlaka za serikali za mitaa kutokana na wahitimu hao kukidhi vigezo vya
kuwasimamia wananchi hivyo ni wajibu wa serikali kuwapatia ajira ili kuleta
ufanisi katika kazi hasa katika wizara hiyo.
Aidha Jafo ameahidi
kukisimamia chuo hicho ili kiweze kutoa wahitimu walio na uelewa mkubwa katika
suala la usimamizi wa mambo mbalimbali ya kijamii ikiwa ni pamoja na
kuhakikisha kinatoa elimu kuanzia ngazi ya astashahada ,stashahada na shahada.
Kwa upande wake
mwenyekiti wa bodi ya udhamini wa chuo hicho prof Suleimani Ngwale amewataka
wanafunzi wote wanaohitimu katika chuo hicho kutumia mnara huo kujipima na
kuenzi matendo yanayofanywa na Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt John
Pombe Magufuli kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.
Naye mkuu wa chuo
hicho dokta Mpamila Madale ameahidi kuyatekeleza mambo muhimu yote
yaliyoelekezwa na serikali ili kuendelea kuboresha chuo hicho.
Na
Alfred Bulahya Dodoma
FM
Comments
Post a Comment