Skip to main content

KATAZO LA RAIS KUTORUHUSU MWANAFUNZI ALIEPATA MIMBA KUENDELEA NA MASOMO LIPO KWA MUJIBU WA SHERIA

                                          Image result for NAIBU WAZIRI WA ELIMU OLE NASHA




Naibu Waziri wa elimu sayansi na teknolojia Mh. William Tate Ole Nasha amesema katazo la wanafunzi waliobebeshwa ujauzito kutokurudi shuleni lipo kwa mujibu wa sheria na Rais ameshalitolea msisitizo.

Mh. Ole Nasha ameyasema hayo leo Bungeni Mjini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge Suzan Limo alietaka kujua Serikali imeshafanya tathimini kuona ni athari gani za kijamii, kiuchumi pamoja na kisaikolojia kwa watoto wanaozaliwa na mabinti hao ambao ni wanafunzi.

Amesema katazo hilo limekuwepo tangu mwaka 2002 kwa mujibu wa kanuni iliyoanzishwa kipengele cha 60, ya sheria ya elimu ya mwaka 1978 na maelekezo yaliyotolewa na Rais Dr. John Pombe Magufuli hivi karibuni ya wanafunzi hao kutokurudi shuleni ni kusisitiza juu ya katazo hilo.

Naibu Waziri Ole Nasha amesema Serikali imechukua uamzi huo ili kumlinda mwanafunzi aliebebeshwa ujauzito kuepuka kunyanyaswa na wanafunzi wengine kutokana na hali aliyo nayo sambamba na kuonesha ni jinsi gani Serikali haiwezi kuendelea kuhudumia mwanafunzi aliebebeshwa ujauzito.

Aidha amesema Serikali inatambua tatizo la wanafunzi hao kubebeshwa mimba wakiwa masomoni kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo zile wasizoweza kuzihimili kama kubakwa, kutembea umbali mrefu kwenda shule, mila na desturi potofu pamoja na kukosekana kwa mahitaji ya msingi kutoka kwa wazazi na kwamba Serikali imeanza mikakati mbalimbali ya kutatua changamoto hizo.

Na Pius Jayunga                                           Bunge/Dodoma FM

Comments