Skip to main content

WANAUME WASHAURIWA KUTOA TAARIFA WANAPOFANYIWA UKATILI.



                             Image result for UKATILI KWA WANAUME

Wanaume mkoani Dodoma wameshauriwa kuwa na desturi ya kutoa taarifa katika vyombo vinavyosimamia masuala ya ukatili, pindi wanapofanyiwa ukatili ili kuendelea kutokomeza ukatili katika jamii.

Kauli hiyo imetolewa leo na mwanasheria kutoka katika taasisi ya sheria ya DARWINS ATORNEY AND CONSULTANTS ya mjini Dodoma bw Chrispin Nicholaus Rwila wakati akizungumza na kituo hiki ofisin kwake.

Amesema kuwa wanaume wengi wamekuwa hawana desturi ya kutoa taarifa kwa vyombo husika pindi wanapofanyiwa ukatili, kutokana na kuogopa fedheha jambo ambalo linaweza kusababisha madhara makubwa kama msongo wa mawazo na hata kifo.

Akizungumzia sheria inayosimamia suala la ubakaji amesema kuwa sheria hiyo haijaweka wazi namna ya kuwasaidia wanaume pindi wanapokumbwa na tatizo hilo, ambapo ameiomba serikali kulitazama jambo hilo kwa jicho la tatu ili kuweka usawa kwa wananchi wote.

Nao baadhi ya wakazi wa mji wa Dodoma wameiambia Dodoma Fm kuwa suala la wanaume kutotoa taarifa pindi wanapofanyiwa ukatili, linatokana na baadhi yao kuona aibu kutokana na kujijengea mazingira ya kuamini kuwa mwanaume ndiyo kichwa cha familia, hivyo akionekana anatoa taarifa za kufanyiwa ukatili anaweza kufedheheka.

Na Alfred Bulahya                                                                   DODOMA FM

Comments