Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imezindua mradi wa kuzuia
maambukizi ya VVU na Ukimwi kwa wasichana balehe na wanawake vijana leo Mkoani
Singida kwa lengo la kuutambulisha kwa jamii kuhusu wasichana na wanawake
vijana walio shuleni na walio nje ya mfumo wa Elimu.
Mradi huu unatekelezwa
na Wizara pamoja na wadau wa Maendeleo kutoka AMREF, TAYOA, na
TACAIDS na Mfuko wa Kimataifa wa Global Fund na wakati huu mradi uko katika
hatua ya majaribio katika mikoa mitatu ya Tanzania ambayo ni Singida, Dodoma na
Morogoro.
Akiongea wakati wa
ufunguzi wa mradi huu leo mjini Singida Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw. Marcel Katemba amesema Wizara
yake imepewa jukumu la kuandaa mazingira rafiki na wezeshi ya utekelezaji wa
Mradi huo na ndiyo maana hatua ya awali ya maandalizi inaanzia kwa kujenga
uwezo kwa wataalamu wa maendeleo ya Jamii kutoka mikoa ya majaribio ya mradi.
Aidha Bw. Katemba
amesema Serikali ya Tanzania imepata ruzuku kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Global
Fund kwa ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali ya mapambano dhidi ya Maambukizi
ya Virusi vya Ukimwi Nchini kwa kipindi cha January 2018
mpaka Desemba 2020.
Nae Naibu Meya wa Mkoa wa Singida Bi. Yagi
Kiaratu amesema maambukizi ya virusi vya Ukimwi katika Mkoa Singida bado ni
Changamoto kubwa na kusema kuwa ujio wa mradi huu mkoani kwake utachangia
kupunguza kuenea kwa virusi hivyo kwa wasichana balehe na wanawake vijana kwa
kupunguza au kutokomeza kabisa ugonjwa huo.
Bi. Yagi ameongeza
kuwa tatizo kwa wasichana wengi walio katika rika hilo wanaingia katika janga
la ukimwi kwasababu bado wanakuwa hawana uelewa wa kutosha kuhusu janga hili
lakini pia wanakuwa hawajaanza kujitambua kama wako katika hatari ya kupata
maambukizi ya ukimwi.
Nao viongozi wa
dini Sheikh Issa Ramadhani simba na mchungaji Felix Kibiriti wameishukuru
serikali kwa mradi huo na kuahidi kuunga mkono kwa kutoa elimu juu ya
maambukizi ya ukimwi katika sehemu za ibada.
Jitihada za kupambana
na ugonjwa wa Ukimwi zimekuwa zikiendelea kwa kipindi cha miongo mitano lakini
kwa kuwa tatizo hili changamoto kwa maendeleo ya Familia na Taifa serikali
inaendelea kuokoa maisha ya watu hasa kwa vijana ambao ndio waathirika wakuu.
Mariam Matundu DODOMA FM
Comments
Post a Comment