Serikali imeombwa kuimarisha kanuni za kuzuia matumizi ya
sigara na tumbaku ili kuendelea kulinda afya za wananchi hapa nchini.
Hayo yamebainishwa na Rais wa chama cha wanafunzi wa famasia
Tanzania (TAPSA) Erick Venant wakati akitoa elimu kuhusu madhara ya tumbaku kwa
wanafunzi wa shule ya sekondari K Ndege iliyopo jijini Dodoma.
Amesema kuwa ni wakati sasa wa jamii kuachana na matumizi ya sigara na
tumbaku kwani kwa sasa magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya tumbaku
yameongezeka.
Ameongeza kuwa licha ya tumbaku kuwa zao la biashara
linalochochea uchumi nchini,watumiaji wake wana uwezekano mkubwa wa kupata
magonjwa ya moyo ,saratani ya mapafu na kifua kikuu.
Rais huyo amesema kuwa wanawake wajawazito wanaovuta sigara
wako katika uwezekano mkubwa wa kujifungua watoto njiti au wenye uzito mdogo
huku akidai kuwa uvutaji wa sigara
majumbani unaweza kuwaathiri wanafamilia na kusababisha kutumia fedha
nyingi katika matibabu.
Kwa upande wake mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo Furaha
kalinga amesema kuwa baadhi ya wanafunzi wenye umri kati ya miaka 13 na 15 wapo
hatarini kutokana na kujaribu kujiingiza katika matumizi hayo licha ya kuelezwa
kuhusu madhara yatokanayo na tumbaku.
Na Alfred Bulahya DODOMA
FM
Comments
Post a Comment