.jpg)
Katika kuelekea Maadhimisho ya siku ya uchangiaji damu Duniani ambayo
huadhimishwa kila mwaka June 14 jamii imeomba kupewa elimu ili waweze kuondokana na imani potofu walizonazo juu ya
uchangiaji damu.
Wakizungumza na Dodoma fm baadhi ya wananchi wamesema
kitengo cha damu salama kimekuwa hakitoi elimu kwa wananchi na badala yake
kimelenga kutoa elimu mashuleni kitendo ambacho hupelekea wachangiaji damu
wengi kuwa wanafunzi.
Kutokana na wananchi kutokupata elimu ya uchangiaji damu hii
imepelekea kuwepo kwa mtazamo hafifu juu ya swala la kuchangia damu ambapo
wengi wao wamekuwa wakidhani uchangiaji wa damu unaweza kumpelekea mwanachama
kuishiwa damu.
Akizungumzia juu ya vigezo vya uchangiaji damu msimamizi mkuu
wa kitengo cha damu salama Jijini Dodoma Dokta Leah Kitundya amesema ili mtu
aweze kuchangia damu ni lazima awe na uzito usipungua Kilo 50 na asiyekuwa na magonjwa nyemelezi.
Aidha amesema mbali na damu kuokoa maisha mchangiaji anaweza
kufahamu afya yake kuwa salama kwa kigezo cha kuchangia damu,kupata cheti cha
uanachama pamoja na kujifahamu kuwa yupo
kundi gani la damu .
Maadhimisho ya uchangiaji damu kwa
mwaka huu yatafanyika uwanja wa Mwalimu nyerere jijini Dodoma yakiwa na
lengo la kutoa zawadi kwa washiriki
ambao wamekuwa wakichangia damu pamoja na kutoa elimu kwa jamii juu ya
uchangiaji wa damu.
Na ANIPHA RAMADHANI DODOMA
FM
Comments
Post a Comment