Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii jinsia wazee na watoto imetoa
tahadhari kwa Wananchi wa Tanzania juu ya Ungonjwa wa Ebola hasa katika mikoa inayopakana na nchi Jirani
ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Akiongea na Waandishi wa Habari mapema leo mjini Dodoma Waziri wa Afya maendeleo ya jamii
jinsia wazee na watoto Mh. Ummy Mwalimu amesema Tanzania inapakana na Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo hivyo ipo hatarini kuambukizwa ugonjwa huo kutokana na
mwingiliano wa watu hasa wasafiri wanaotoka na kuingia nchini.
Waziri Ummy ameitaja mikoa inayopakana na Nchi hiyo kuwa ni Mwanza,
Kagera, Kigoma, Katavi, Rukwa na Songwe.
Amesema ugojwa wa Ebola husababishwa na virusi vya Ebola ambavyo
huambukiza kwa njia ya kugusa damu au majimaji kutoka kwa mtu aliyeambukizwa
ugonjwa huo, kugusa maiti ya mtu aliyekufa kwa ugonjwa huo pamoja na kugusa
wanyama walioambukizwa.
Akizitaja dalili za ugonjwa wa Ebola Waziri Ummy amesema huanza
kuonekana kwa mtu aliyeambukizwa baada ya siku 2 hadi 21 tangu kupata
maambukizi na kwamba mtu atakuwa na homa
kali ya ghafla, kulegea kwa mwili, maumivu ya misuli pamoja na kuumwa kichwa na
vidonda kooni.
Sambamba na hayo amesema ili kujikinga na ugonjwa huo ni kuepuka
kugusa au kuingiwa na mate, damu, mkojo, kinyesi, machozi na majimaji mengine
yanayotoka katika mwili wa mtu mwenye dalili za ugonjwa huo.
Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu bali kuendelea kuchukua
tahadhari za kujikinga na ugonjwa huo na kwamba mpaka sasa hakuna mtu
aliyethibitishwa kuugua ugonjwa huo hapa nchini.
Na Phina Nimrod Dodoma FM
Comments
Post a Comment