Rai imetolewa kwa
wanahabari kushiriki katika kujenga jukwaa la habari lenye maslahi na tija
baina yao na Serikali ili kuondokana na kuwekeana mashaka baina ya pande hizo
mbili.
Rai hiyo imetolewa
na Waziri wa Habari Sanaa Utamaduni na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe wakati
akizungumza katika Kongamano la Maadhimisho ya kilele cha uhuru wa Vyombo vya
habari yaliyofanyika katika ukumbi wa Morena Jijini Dodoma .
Waziri Mwakyembe amesema
ni vyema kujenga maslah kwa pande zote ili kuondokana na mashaka ambayo Wanahabari
na serikali wanawekeana.
Awali Mwenyekiti wa MISA Tanzania ambao ndio
waratibu wakuu wa Maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya habari Bi. Salome Kitomari amesema kumekuwa na
ongezeko la matukio ya kutekwa na kuteswa kwa wanahabari ikiwemo la kupotea kwa
mwandishi wa Gazeti la Mwananchi Azory Gwanda aliyetoweka mnamo mwezi
Novemba mwaka jana.
Bi Kitomari
ameitaka Serikali kupitia jeshi la Polisi liwatafute na kuwachukulia hatua
waliotenda tukio hilo.
Aidha Kaimu
Mwenyekiti kutoka jukwaa la wahariri Tanzania Deodatus Balile amesema Uhuru wa
Habari Tanzania umebainika kuzorota huku mazingira ya wanahabari kuwa ya
hofu kutokana na kuwepo kwa vitendo vya unyanyasaji ikiwemo kunyang’anywa
vitendea kazi.
Kwa upande wake
makamu wa Rais wa Klabu za waandishi wa
habari nchini Tanzania UTPC Bi. Jane Mihanje ameiomba Serikali kupanua wigo wa
uhuru wa vyombo vya Habari na kuwalinda kutokana na kuwa waoga kwa matukio
yanayoendela juu ya Waandishi wa Habari.
Na Phinna Nimrodi Dodoma FM
Comments
Post a Comment