
Wafanyabiashara
wa soko la Sabasaba jijini Dodoma wameulalamikia uongozi wa soko hilo
kuwahamisha mara kwa mara na kuwapeleka katika eneo ambalo sio rafiki kwa
kufanyia biashara.
Wametoa
malalamiko hayo mapema hii leo wakati wakizungumza na Dodoma FM kupitia kipindi cha Taswira ya habari ambapo wamedai kuwa uongozi wa soko hilo umekuwa na tabia ya kuwahamisha
mara kwa mara na kuwapeleka mahali ambako hakuna miundo mbinu rafiki hali inayowalazimu
kufanya biashara katika milango ya
maduka ya wafanyabiashara wa nguo na kusababisha ugomvi baina yao.
Akijibu
malalamiko hayo mwenyekiti wa soko hilo Bwana Athumani Makole amekanusha suala la wafanyabiashara hao kuhamishwa katika eneo lao
ambapo amedai kuwa baadhi yao wamekuwa wakifanya hivyo wao wenyewe na ndipo uongozi unapowataka kurudi katika maeneo yao huku wao wadai kuwa wanafukuzwa.
Katika hatua nyingine
Taswira ya habari imezungumza na mwenyekiti wa Soko kuu Majengo, jijini Dodoma Bwana Godson Lugazama
ambapo ameuomba Uongozi wa Jiji kukarabati miundombinu ya soko hilo iliyo
chakavu pamoja na kuongeza ukubwa wa soko kutokana na ongezeko la watu mbalimbali
wanaoendelea kuingia mkoani hapa.
Lugazama amebainisha kuwa
miundombinu hiyo imechakaa hususani mapaa na hivyo wakati wa kipindi cha masika
mapaa huvuja jambo ambalo ni kero kwa wafanyabiashara wa soko hilo.
Soko kuu la Majengo
limejengwa tangu mwaka 1996 na linadiawa kuwa na Zaidi ya wafanyabiashara 400
wanaolipa ushuru.
Na Alfred Bulahya DODOMA
FM
Comments
Post a Comment