Serikali imeombwa kutoa
ushirikiano kwa vyombo vya habari nchini ili kuendelea kutokomeza vitendo viovu
katika maeneo mbalimbali ambavyo vimekuwa vikichangia kukwamisha maendeleo ya
Taifa.
Kauli
hiyo imetolewa leo jijini Dodoma na Makamu wa Rais wa Klabu za waandishi wa
habari Tanzania (UTPC) Bi Jane Mihanji wakati akizungumza na waandishi wa
habari kuelekea maadhimisho ya siku ya vyombo vya habari ambayo yanatarajiwa
kufanyika kitaifa Mei 2 na Mei 3 mkoani hapa.
Amesema
kuwa kumekuwepo na baadhi ya viongozi mbalimbali ambao wamekuwa wakijenga chuki
kwa waandishi wa habari kutokana na waandishi hao kuandika habari zinazofichua
maovu yanayofanywa na viongozi hao jambo ambalo linakwamisha maendeleo ya taifa
ikiwemo kuwanyima haki wananchi kupata habari.
Katika
hatua nyingine Bi Mahinji amewaomba wamiliki wa vyombo vya habari nchini
kuhakikisha wanazingatia utoaji wa ajira kwa mikataba na kuboresha masilahi ya
wafanyakazi wao kwani waandhishi wa habari wamekua wakifanya kazi kubwa ikiwa
ni pamoja na kuisukuma serikali kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu.
Kwa
upande wake mratibu kutoka Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Bwana Neville
Meena amesema kuwa jukumu la kupata habari sio la waandishi wa habari pekee
bali hata wananchi wana haki ya kudai taarifa kwa kiongozi yeyote hivyo ni vyema jamii ikatambua jambo hilo ili
kuunga mkono jitihada zinazofanywa na waandishi wa habari.
Bi
Raziah Mwawanga ambaye ni wakfu wa vyombo vya habari amesema kuwa umefika
wakati sasa wa waandishi wa habari kutumia vizuri kalamu zao kwa kuandika
habari bila kumuonea mtu yeyote ili kupunguza changamoto zinazoikumba tasnia
hiyo.
Siku
ya uhuru wa vyombo vya habari huadhimishwa kila mwaka ifikapo may 2 na kwa
mwaka huu yataadhimishwa jijini Dodoma yakiwa na kauli mbiu isemayo wajibu wa serikali , vyombo vya habari, haki na
utawala wa sheria.
Na Alfred Bulahya. Dodoma FM
Comments
Post a Comment