Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto imedhamiria kumlinda mtoto dhidi ya ukatili ukiwemo unyanyasaji
wa mtandaoni.
Katika kulifanikisha hilo Wizara imekutana na wadau wa maendeleo
ya mtoto Jijini Dodoma kujadili kuhusu namna bora ya kupambana na ukatili wa
mtoto mtandaoni ambao unaenea kwa kasi kubwa na kutishia hatima ya watoto na
jamii kwa ujumla.
Akifungua kikao kati ya Serikali na wadau wa Maendeleo ya Mtoto
Kaimu Katibu Mkuu Idara Kuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bw.
Marcel Katemba amesema kuwa Serikali haitafumbia macho matumizi ya mitandao
ambayo yana athari mbaya kwa watoto ili kuhakikisha kuwa kunakuwepo udhibiti wa
matumizi ya mitandao ili kuwalinda watoto dhidi ya unyanyasaji wa kingono mtandaoni.
Bw. Marcel Katemba ameleza kuwa Serikali inatambua mchango wa
wadau katika mapambano dhidi ya ukatili wa kingono kwa watoto mitandaoni, hivyo
kwa pamoja watashirikiana kuhakikisha kuwa vita ya kupambana na ukatili dhidi
ya Mtoto ikiwemo ukatili wa mtandaoni inafanikiwa.
Ameongeza kuwa Serikali inatambua mchango wa wadau katika ulinzi
na usalama wa watoto na Serikali itaendelea kushirikiana na wadau ili kupata
mbinu na namna sahihi za kupambana na ukatili ili kulinda watoto wetu dhidi ya
madhara ya matumizi maovu ya mitandao.
Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo cha Ualimu Dar es
salaam (DUCE) Dkt. Hezron Onditi akiwasilisha utafiti kuhusu hali ya ukatili wa
mtoto mtandaoni, amesema kuwa tatizo la ukatili wa mtandaoni kwa watoto ni
kubwa na linaenea kwa kasi na mpaka sasa takribani asilimia ya 5 – 72 ya watoto
na vijana wadogo duniani wamefanyiwa ukatili wa kingono mtandaoni
ikilinganishwa na asilimia 58 ya watoto waliofanyiwa ukatili huo kupitia
matumizi ya simu na mitandao hapa nchini.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto Bi. Magreth Mussai
amesisitiza kuwa wazazi na walezi na jamii kwa ujumla wanatakiwa kuzingatia na
kuimarisha malezi ya watoto katika mazingira ya shule na majumbani ili kuzuia athari mbaya
zinazosababishwa na matumizi mabovu ya simu na mitandao katika dunia ya
teknolojia na utandawazi.
MARIAM MATUNDU DODOMA
FM
Comments
Post a Comment