
Serikali
imesema katika kipindi cha Januari hadi mwezi Desemba mwaka 2017 Jeshi la
polisi Nchini limeripoti kupokea matukio yapatayo 41,416 ya vitendo vya ukatili
wa kijinsia kwa wanawake na watoto.
Naibu
Waziri wa afya maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto Dr. Faustine Ndugulile
ameyasema hayo leo Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali namba 49 la Mbunge
wa viti maalumu Mwatumu Dau Haji aliehoji juu ya takwimu za matukio ya ukatili wa
kijinsia kwa wanawake na watoto.
Naibu Waziri wa Afya amesema
kati ya matukio hayo, matukio 13,457 ni ya ukatili wa kijinsia kwa watoto
kitendo ambacho Serikali imekuwa ikihakikisha inayatokomeza huku jamii
ikitakiwa kutoa taarifa mapema katika vyombo vya sheria pale matukio hayo
yanapojitokeza.
Kutokana
na takwimu hizo Dr. Ndugulile amekiri kuongezeka kwa matukio ya ubakaji na
ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto na katika kukabiliana na tatizo hilo
Serikali kwa kushirikiana na wadau imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuzindua
mpango wa Taifa wa miaka mitano wa mwaka 2017/18 hadi 2020/21/22 wa kutokomeza
ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.
Dr. Ndugulile amesema kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi
kujitokeza kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia kumechangiwa na ongezeko la
ukubwa wa tatizo hilo na kutokana na changamoto hiyo Dr. Ndugulile amewataka
wananchi kuacha utamaduni wa kutatua migogoro hiyo katika ngazi ya familia
badala yake taarifa hizo zifikishwe moja kwa moja katika vyombo vya sheria.
Na Pius Jayunga DODOMA FM
Comments
Post a Comment