Naibu
Waziri wa elimu sayansi na teknolojia Mh. William Tate Ole Nasha amesema katazo
la wanafunzi waliobebeshwa ujauzito kutokurudi shuleni lipo kwa mujibu wa
sheria na Rais ameshalitolea msisitizo.
Mh.
Ole Nasha ameyasema hayo leo Bungeni Mjini Dodoma wakati akijibu swali la
Mbunge Suzan Limo alietaka kujua Serikali imeshafanya tathimini kuona ni athari
gani za kijamii, kiuchumi pamoja na kisaikolojia kwa watoto wanaozaliwa na
mabinti hao ambao ni wanafunzi.
Amesema
katazo hilo limekuwepo tangu mwaka 2002 kwa mujibu wa kanuni iliyoanzishwa
kipengele cha 60, ya sheria ya elimu ya mwaka 1978 na maelekezo yaliyotolewa na
Rais Dr. John Pombe Magufuli hivi karibuni ya wanafunzi hao kutokurudi shuleni
ni kusisitiza juu ya katazo hilo.
Naibu
Waziri Ole Nasha amesema Serikali imechukua uamzi huo ili kumlinda mwanafunzi
aliebebeshwa ujauzito kuepuka kunyanyaswa na wanafunzi wengine kutokana na hali
aliyo nayo sambamba na kuonesha ni jinsi gani Serikali haiwezi kuendelea kuhudumia
mwanafunzi aliebebeshwa ujauzito.
Aidha
amesema Serikali inatambua tatizo la wanafunzi hao kubebeshwa mimba wakiwa
masomoni kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo zile wasizoweza kuzihimili kama
kubakwa, kutembea umbali mrefu kwenda shule, mila na desturi potofu pamoja na
kukosekana kwa mahitaji ya msingi kutoka kwa wazazi na kwamba Serikali imeanza
mikakati mbalimbali ya kutatua changamoto hizo.
Na Pius Jayunga Bunge/Dodoma FM
Comments
Post a Comment