Zaidi ya hati miliki Elfu nne (4000) za kimila zinazohusisha umiliki wa
ardhi zinatarajiwa kutolewa na shirika la Pelum Tanzania katika
vijiji 30 nchini.
Maeneo yatakayohusika na hati hizo ni Wilaya za Mvomero, Morogoro, Kilolo, Mufindi, Bahi pamoja na
Kongwa ili kufanikisha mpango wa matumizi bora ya ardhi vijijini.
Hayo yamebainishwa leo na afisa mradi wa Ushiriki wa
Wananchi katika Kusimamia Sekta ya ardhi na Kilimo, kutoka shirika la PELUM
TANZANIA Bi Anna Marwa wakati akizungumza katika mdahalo maalumu
wilayani Bahi Mkoani Dodoma uliowakutanisha viongozi mbalimbali wakiwemo madiwani na
wenyeviti wa vijiji wenye lengo la kutambua usimamizi wa mpango wa matumizi sahihi
ya ardhi.
Amesema kuwa June Mwaka huu Mradi huo unatarajia kufikia
tamati, na unamalizika ukiwa umeacha mabadiliko makubwa katika vijiji 30 vya
wilaya hizo ambapo mbali na kutoa hati miliki kwa wananchi hao mradi huo
umeweza kutatua migogoro ya ardhi kwa kiasi kikubwa huku asilimia 30
ukiwasaidia wananchi kunufaika na uelewa juu ya masuala ya ardhi.
Awali akifungua mdahalo huo mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya
ya Bahi ambaye ni diwani wa kata ya Mwitikia Bwana Danford Chisomi amewataka
wananchi kutumia mafunzo hayo kujiletea maendeleo kupitia fursa ya umiliki wa
ardhi huku akiwataka wenyeviti wa vijiji kusimamia kikamilifu majukumu yao
ikiwa ni pamoja na kuendelea kutatua migogoro ya ardhi ili kufikia malengo
mahususi yaliyokusudiwa.
Nao baadhi ya wananchi walionufaika na mradi huo wamelishukuru
shirika hilo kwa kutoa mafunzo hayo na kuahidi kuwa chachu ya kuleta maendeleo
katika jamii kwa kutoa mafunzo kwa wananchi wengine ili kukomesha migogoro ya
ardhi ambayo imekuwa ni tatizo kubwa hapa nchini.
Mnamo mwaka 2013 Shirika la PELUM TANZANIA kupitia Ufadhili wa
Shirika la Misaada la Watu wa Marekani, lilianzisha mradi wa Ushiriki wa
Wananchi katika Kusimimia Sekta ya Kilimo, unaojulikana kama CEGO (CITIZEN
ENGANGING IN GOVERNMENT OVERSIGHT) mradi ambao umetekelezwa katika mikoa
Mitatu ya Morogoro, Iringa na Dodoma na unatarajia kufikia kikomo ifikapo june
9 mwaka huu.
Na Alfred
Bulahya. Dodoma
FM
Comments
Post a Comment