Wakala wa usalama
na afya mahala pa kazi nchini (OSHA) iliyopo chini ya waziri wa kazi,vijana,
ajira na watu wenye ulemavu wamezitaka sekata mbalimbali kuzingatia sheria kanuni na
taratibu za usalama na afya mahala pa kazi wakati wakiendesha shughuli zao.
Kauli hiyo
imetolewa mjini Dodoma na mkaguzi wa ujenzi kutoka OSHA kanda ya kati Mhandisi
Robert Mashinji wakati akizungumza na Dodoma FM kuelekea maadhimisho ya kila
mwaka ya siku ya usalama na afya mahala pa kazi yanayotarajia kufanyika kitaifa
mkoani Iringa ifikapo april 28 mwaka huu.
Mashinji amesema
taasisi na wadau mbalimbali wanaojihusisha na utoaji wa huduma mbalimbali kwa
jamii kama vituo vya kuuza mafuta, kumbi
za starehe na zile za mikutano zinapaswa kutambua matumizi sahihi ya vifaa
kinga mahala pa kazi ikiwemo kuweka vifaa vya kudhibiti hatari kama majanga ya
moto katika maeneo yao ya kazi.
Ameongeza kuwa osha
imekuwa ikifanya kazi ya ukaguzi katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu kama
viwanda,migodi, miradi ya ujenzi, benki,
hospitali pamoja na nyumba za kulala wageni
ili kuangalia namna waajiri wanavyowakinga wafanyakazi dhidi ya vihatarishi
mahala pao pa kazi na inapobaini kuwepo kwa ukiukwaji hatua kali huchukulia
ikiwemo adhabu za papo kwa papo au kufikishwa mahakamani.
Aidha bwana
Mashinji amewakumbusha wadau kwa kutaja vifaa vinavyokaguliwa kuwa ni pamoja na
usalama wa mtandao wa umeme, miundombinu ya kujiokoa wakati wa dharura, ubora
wa mazingira ya kufanyia kazi pamoja na usahihi wa vifaa kinga anayopewa
mfanyakazi.
Maadhimisho ya siku
ya usalama na afya mahala pa kazi huadhimishwa duniani kote kila mwaka ifikapo
april 28 na kwa mwaka huu nchini Tanzania yataadhimishwa kitaifa mkoani Iringa
yakiwa na kauli mbiu isemayo "kizazi salama chenye afya kwa maendeleo ya
viwanda".
Na Alfred
Bulahya Dodoma FM
Comments
Post a Comment