Rais John Magufuli
amemtaka Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isaac Kamwelwe na Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma, Dk Binilith Mahenge kufuatilia ubadhirifu wa fedha za mradi wa maji
katika Mkoa wa Dodoma na kuhakikisha wahusika wanakamatwa au maji yanatoka.
Rais Magufuli
ameyasema hayo leo Aprili 27, wilayani Kondoa wakati wa hafla ya uzinduzi wa
barabara ya Dodoma – Babati yenye urefu wa kilomita 251 ambayo ni sehemu ya
barabara kuu inayotoka Capetown, Afrika Kusini mpaka Cairo, Misri.
Ameagiza vyombo vya
dola kuwatafuta wahusika wa ubadhirifu wa fedha hizo ambazo amesema ni zaidi ya
Sh2 bilioni.
Amesema ni lazima
wahusika wachukuliwe hatua kwa sababu hizo ni fedha za wananchi, na ni vyema
ziwaletee maendeleo.
“Haiwezekani tukawa
tunaimba maji kila siku halafu maji hayatoki. Vyombo vya dola vihakikishe
wahusika wote wanakamatwa au maji yanatoka. Tukibembelezana hivi hatutafika,
hata hii barabara tusingebana, isingekamilika,” amesema Rais Magufuli.
Awali kabla ya Rais
Magufuli kuzungumza, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge alisema kuna
ubadhirifu wa Sh1.5 bilioni kwenye mradi wa maji katika wilaya za Kondoa na
Chemba ambao mpaka sasa unasuasua.
Mkuu huyo wa mkoa
alisema mradi huo ulitengewa Sh2.8 bilioni kwa ajili ya wilaya hizo,
lakini kulitokea ubadhirifu wa Sh1.5 bilioni.
Amebainisha kwamba
vyombo vya dola vinaendelea na uchunguzi wa ubadhirifu huo.
Na Zania Miraji Dodoma FM
Comments
Post a Comment