Wahitimu wa kidato
cha sita katika shule ya sekondari Dodoma wametakiwa kuhakikisha wanaitumia
vizuri elimu waliyoipata kwa kuwa mabalozi wakubwa katika kusaidia ujenzi na
ustawi wa taifa ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Kauli hiyo
imetolewa leo na Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira, ambae pia ni
mbunge wa jimbo la Dodoma Mjini Mhe. Anthony Mavunde wakati
akitoa hotuba kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Dodoma katika mahafali ya 15 ya kidato cha sita.
Mavunde Amesema
kuwa wahitimu hao wanatakiwa kuwa mabalozi wazuri kwenye jamii katika kutoa
elimu juu ya maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi pamoja na madhara ya matumizi ya
madawa ya kulevya ambayo yamekuwa yakichangia kuongeza kundi kubwa la watu
wenye utegemezi.
Awali akisoma
risala mbele ya mgeni rasimi mkuu wa shule ya sekondari Dodoma AMANI MFAUME ameiomba serikali
kuhakikisha inatatua changamoto ya upungufu wa mabweni kwa ajili ya wanafunzi
wa kiume kwani jambo hilo limekuwa likisababisha baadhi ya wanafunzi kupanga vyumba
mitaani hali ambayo inawafanya kukosa usimamizi katika masomo na kusababisha
kuwa na ushiriki hafifu kwenye masomo yao.
Amesema mbali na
hilo baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakijikuta wakiingia katika vishawishi
mbalimbali vya kuishi katika maisha ya kimjini na kusababisha matokeo yao kuwa
mabaya ukilinganisha na upande wa wasichana ambao wanaishi ndani ya eneo la
shule.
Naibu waziri Mavunde ameahidi kuhakikisha changamoto hizo
zinatatuliwa katika shule hiyo ili kuwajengea uwezo mkubwa wa kitaaluma
wanafunzi hao.
Na
Alfred bulahya Dodoma
FM
Comments
Post a Comment