ZAIDI YA WANAFUNZI MIA NANE WALIOFAULU KUJIUNGA KIDATO CHA KWANZA MJINI DODOMA HAWAJARIPOTI SHULENI MPAKA SASA
Wito
umetolewa kwa wazazi na walezi katika manispaa ya Dodoma kuwapeleka shule
wanafunzi waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza kabla ya tarehe ya mwisho
iliyopangwa.
Wito huo umetolewa
na Afisa elimu sekondari wa manispaa ya Dodoma ABDALLAH MEMBE wakati akizungumza na Dodoma FM
kupitia kipindi cha Taswira ya Habari juu ya tathmini ya wanafunzi ambao ambao
tayari wameripoti shuleni mpaka sasa.
Bwana Membe amesema
kuwa baadhi ya wazazi na walezi hushindwa kuwapeleka wanafunzi kidato cha
kwanza kwa sababu zisizo za msingi na hivyo kumnyima mtoto haki yake ya msingi.
Bwana MEMBE amesema
kuwa kutokana na baadhi ya wazazi kuwa na
muamko mdogo wa elimu wamekuwa wakiwanyima watoto wao fursa ya kuendelea
na masomo pindi wanapohitimu elimu ya
msingi na badala yake huwasafirisha katika mikoa tofauti kwenda kufanya kazi za
ndani huku wengine wakibaki nyumbani na kufanya shughuli za kilimo na kuchunga
mifugo.
Aidha afisa huyo amebainisha
kuwa kutokana na jumla ya wanafunzi 6559 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha
kwanza katika shule 37 za serikali manispaa ya Dodoma kwa mwaka huu ni
wanafunzi 5710 ambao tayari wameanza shule huku wakisalia wanafunzi 849 ambao
hawajaripoti kwenye shule walizopangiwa mpaka sasa.
Hata hivyo
amewataka wazazi na walezi kutoa taarifa pale mwanafunzi anapoanzishwa kidato
cha kwanza katika shule binafsi kwani kutofanya hivyo ni kosa kisheria na
adhabu kali huchukuliwa dhidi ya anayekiuka masharti.
Na
RWEIKIZA KATEBALIRWE DODOMA FM
Comments
Post a Comment