Waajiri wa walimu katika shule
za Msingi na Sekondari za umma kote Nchini wakiwemo wakurugenzi wa halmashauri
za Wilaya, Manispaa na Miji, wametakiwa
kufuata sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma katika utoaji wa vibali
vya ruhusa kwa walimu.
Katibu wa tume ya
utumishi wa walimu Nchini Bi. Winifrida Rutaindurwa ametoa maagizo hayo leo
wakati akizungumza na vyombo vya habari ofisini kwake Mjini Dodoma ambapo
amesema kumekuwa na mazoea ya waajiri kutoa ruhusa ya mdomo au makubaliano kwa njia ya simu jambo ambalo ni
kinyume na utaratibu.
Aidha amekemea
tabia ya baadhi ya walimu Nchini kuondoka katika vituo vyao vya kazi kwenda
masomoni bila kibali cha mwajiri na kibali hicho kinatakiwa kuwa katika
maandishi huku akiwataka walimu kuzingatia muda wa kurudi katika vituo vyao vya
kazi mara baada ya kuhitimu masomo yao.
Ameongeza kuwa
maafisa elimu Nchini wanapaswa kutambua majukumu yao kuwa ni pamoja na
kuwashauri waajiri wa walimu katika halmashauri na kwamba ni wajibu wao
kuhakikisha walimu wa shule za msingi na sekondari za umma wanahudumiwa kwa
kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Nchi.
Kwa upande wake
afisa sheria wa tume ya utumishi wa walimu Nchini Wakili Deogratius Osmasi
Haule amesema ni kosa kisheria kwa mwalimu kuondoka katika kituo chake cha kazi
bila kibali cha mwajiri ikiwa ni pamoja na ruhusa hizo kuwa katika mfumo wa
maandishi huku mwajiri akitakiwa kutoa ruhusa mapema ili kuepusha madhara
ambayo huwenda yakatokea kwa mwalimu ikiwemo kushushwa kazi, kushushwa mshahara
pamoja na kufukuzwa kazi.
Na
Pius Jayunga
Dodoma FM
Comments
Post a Comment