Wanachama wa Chama
cha Mawakili Tanganyika (TLS) wameshauriwa kutumia nafasi waliyo nayo
kuipongeza, kuikosoa na kuishauri serikali katika utendaji kazi wake, ili
kuisaidia kupigania rasilimali za nchi .
Kauli hiyo
imetolewa leo na mgombea urais wa chama cha mawakili Tanganyika (TLS) Bwana
Godfrey Wasonga wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kuwa
chama hicho kinapaswa kusimama kidete katika kuisaidia serikali kupigania
rasilimali za nchi kwa manufaa ya Taifa.
Amesema kuwa
serikali ilitunga sheria yenye kuwapa uwezo mawakili kuhakikisha wanaipongeza
serikali inapofanya vizuri pamoja na kuikosoa inapokwenda kinyume na taratibu
hivyo ni jukumu la kila mwanasheria hapa nchini kuisaidia serikali katika
kupigania haki za wananchi.
Akieleza mikakati
yake Wasonga amesema endapo atachaguliwa
kukiongoza chama hicho katika ngazi ya urais atashawishi kuongezwa nafasi
mbalimbali za uwakilishi katika chama hicho kama kuongeza nafasi mbili za
wakina mama,nafsi mbili za vijana pamoja na nafasi ya mtu mmoja kwa upande wa
watu wenye ulemavu ili kuboresha utendaji kazi wa chama hicho.
Aidha ameongeza
kuwa katika kuendelea kukiboresha chama hicho juhudi mbalimbali zinahitaji
kufanyika ili kukiondoa chama hicho katika hali ya utegemezi kwa kuanzisha
miradi mbalimbali itakayowasaidia mawakili kuhudumiwa kwa wakati na kwa ufasaha
pindi wanapopatwa na matatizo.
Chama cha
Wanasheria Tangangika law society (TLS) kinatarajia kufanya uchaguzi kwa nafasi
mbalimbali za uongozi kuanzia mwezi April mwaka huu ambapo Godfrey Wasonga
ametangaza nia ya kugombea Urais.
Na
Alfred Bulahya
Dodoma FM
Comments
Post a Comment