Mwenyekiti wa shirikisho la
vyama vya tiba asili Tanzania amesema shirikisho hilo halitasita kumchukulia
hatua za kisheria mganga yeyote wa tiba asili atakaejihusisha na kupiga ramli
chonganishi.
Bw. Abdalaman Mussa Lutenga ameyasema hayo
kufuatia Serikali kupitisha matumizi ya dawa za tiba asili zilizo thibitishwa
na mkemia mkuu wa Serikali kuwa zinaweza kutibu tatizo la nguvu za kiume na
hivyo huwenda baadhi ya waganga wakatumia mwanya huo kukiuka sheria za tiba
asili kitendo ambacho hakitavumiliwa.
Amesema sheria ya tiba asili inapinga matumizi
ya tiba zitokanazo na ramli chonganishi ambazo huchangia kwa kiasi kikubwa
kuchonganisha watu na kuvunja sheria namba 23 kifungu cha 30 kinachozuia mganga
kutoa huduma ya tiba asili kwa njia ya ramli.
Bw.Lutenga amesema shirikisho la vyama vya tiba
asili Tanzania litaendelea kuelimisha waganga hao ili kuitambua sheria na
kwamba elimu hiyo imekuwa ikifikishwa kwa waganga katika Mikoa yote Tanzania ili
kuwaepusha kujihusisha katika ramli chonganishi.
Ikumbukwe kuwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na
Watoto, Dk Faustine Ndugulile amekwisha kumuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Afya
akishirikiana na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR),
kufanya utafiti wa afya ya uzazi kwa wanaume ili kubaini sababu za tatizo hilo na
kujua ongezeko la upungufu wa nguvu za kiume ni kubwa kiasi gani nchini.
NA PIUS JAYUNGA DODOMA FM
Comments
Post a Comment