Ukosefu wa vyuo vya ufundi katika Wilaya ya
Kongwa Mkoa wa Dodoma ni moja ya sababu zinazokwamisha vijana wengi Wilayani
humo kuto kufikia malengo yao.
Baadhi ya vijana katika wilaya ya
Kongwa wamebainisha hayo wakati wakizungumza na Dodoma Fm na kueleza kuwa licha
ya wao kuwa na ndoto ya kufanikiwa kwa kujishughulisha na shughuli za ufundi
bado wanakwama kufanikisha malengo yao kutokana na kuto kuwepo kwa vyuo vya
ufundi ambavyo vinaweza kuwaongezea ujuzi zaidi.
Wamesema ni vema Serikali
ikatekeleza ahadi zake kwa wananchi Wilayani humo ikiwemo ujenzi wa vyuo vya
ufundi ili kutoa fursa kwa vijana kupatiwa elimu na ujuzi wa kufanya kazi kwa
maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa
wa Mnyakongo Wilayani Kongwa Bwana Moses Patson amesema ukosefu wa vyuo vya
ufundi umechangia vijana wengi kushinda mitaani na baadhi yao wamekuwa
wakituhumiwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu.
Hata hivyo Mkurugenzi Mtendaji wa
halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Mhandisi Ngusa
Izengo amesema uongozi wa Wilaya unatambua kuwepo kwa changamoto hiyo na
tayari wametoa eneo la ekali 200 kwa jeshi la kujenga Taifa JKT ili kujenga
chuo cha ufundi pamoja na ujenzi wa chuo cha maji kupitia Wizara ya maji.
Na PiusJayunga Dodoma Fm
Comments
Post a Comment