
Baadhi
ya wakazi wa Kata ya Mnyakongo shuleni katika Wilaya ya Kongwa Mkoa wa Dodoma
wamelalamikia ubovu wa eneo la makutano ya barabara ya Mbande, Mpwampwa na
Kongwa.
Wakizungumza na Dodoma
FM wananchi hao akiwemo Jumbe Jarom pamoja na Wilson Batogwa wamesema kutokana
na ubovu wa eneo hilo kunachangia kuwepo kwa ajali za mara kwa mara huku ufinyu
wa eneo hilo wakati wa kupishana magari pamoja na wingi wa mchanga vikitajwa
kuwa ni moja ya sababu za ajali.
Wananchi hao
wamebainisha kuwa kuna ajali ambazo zimewahi kutokea katika eneo hilo na
kupoteza maisha ya watu huku wakilalamikia ukosefu wa alama za usalama barabarani
kuwa ni moja ya chanzo cha kutokea kwa ajali hizo.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mnyakongo shuleni Bw. Moses Patson amekiri kuwepo kwa
changamoto hiyo kwa muda mrefu licha ya kufikisha malalamiko hayo kwa viongozi
wa ngazi za juu lakini bado utekelezaji wake umekuwa mdogo na athari nyingi zikiendelea
kutokea.
Dodoma FM Habbari imezungumza
na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Mhandisi Ngusa Izengo juu ya
changamoto hiyo na kukiri kuwepo kwa ubovu wa makutano ya barabara hizo huku
akieleza kuwa barabara hiyo iko chini ya wakala wa barabara nchini (TANROADS)
na wao kama Halmashauri wamekwisha wasiliana na Tanroads kwa ajili ya
utekelezaji wa zoezi hilo.
Na
Pius Jayunga Dodoma FM
Comments
Post a Comment