Wazazi na walezi wametakiwa kuwa karibu na watoto wao pindi wanapohitimu elimu ya Darasa la saba ikiwa ni pamoja na kuzungumza nao namna ya kuishi na kuepuka vishawishi mbalimbali ikiwemo mimba za utotoni katika kipindi cha kusubiri matokeo.
Akizungumza na Taswira ya habari Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Dawati la Jinsia Bi. Lovie Mhena amesema katika kipindi cha Darasa la saba ndicho kipindi cha ukuaji wa watoto hivyo wazazi wanapaswa kutenga muda wa kuzungumza na mtoto stadi mbalimbali za maisha ili waweze kuwa salama pindi matokeo yanapotoka.

Bi. Lovie amesema kuwa wapo wazazi ambao wamekuwa wakitengemea walimu katika kuzungumza na watoto wao mbinu mbalimbali za kuepukana na vishawishi kutokana na sababu mbalimbali wanazokuwa nazo ikiwemo kubanwa na majukumu ya kikazi hali inayopelekea baadhi ya watoto kupata mimba za utotoni.
Kwa upande wake mzazi Miriam Sauli amewaomba wanafunzi kutambua kwamba elimu ni kitu cha msingi na wanatakiwa kujiandaa kwa kujilinda katika kipindi chote cha kusubiri matokeo ya kuingia kidato cha kwanza.
Bi. Lovie amewataka wanafunzi hao kutokubweteka na kutorubunika na vishawishi wanavyokutana navyo katika kipindi hicho cha kusubiri matokeo na kutambua kuwa wanasafari ndefu katika masomo yao hivyo wajitunze ili kuepuka kukatisha masomo yao kwa kupata mimba.
Comments
Post a Comment